UTANGULIZI/ HISTORIA
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ni chombo cha udhibiti kilichoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410, chenye jukumu la kudhibiti na kusimamia ununuzi wa umma pamoja na masuala yanayohusiana nayo kwa kuzingatia matakwa ya sheria hiyo.
Mamlaka ilianzishwa mwezi Mei, 2005 kufuatia kutungwa kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004, ikiwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wake. Mamlaka ilichukua nafasi ya Bodi Kuu ya Zabuni (Central Tender Board - CTB) iliyokuwa imeanzishwa chini ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2001.
Katika jitihada za kuboresha zaidi sekta ya ununuzi wa umma, Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2011 ilitungwa na kufuta Sheria ya mwaka 2004. Aidha, kutokana na mabadiliko ya mazingira pamoja na hitaji la kuendana na matumizi ya mifumo ya kidijitali, Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 ilitungwa.
MALENGO
Malengo ya Mamlaka kama yalivyoainishwa chini ya Kifungu cha 9 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma ni kama ifuatavyo:
a) Kuhakikisha upatikanaji wa thamani halisi ya fedha katika ununuzi na ugavi;
b) Kuhakikisha uzingatiaji wa misingi ya haki, ushindani, uwazi, uendelevu, uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali katika ununuzi na ugavi;
c) Kuweka viwango vya mifumo ya ununuzi na ugavi wa umma katika Jamhuri ya Muungano;
d) Kuhakikisha kuwa taasisi za ununuzi zinatoa kipaumbele kwa wazabuni wazawa katika ununuzi wa bidhaa, kazi za ujenzi na huduma;
e) Kufuatilia uzingatiaji wa sheria na kanuni za ununuzi na taasisi za ununuzi; na
f) Kujenga uwezo katika masuala ya ununuzi na ugavi kwa kushirikiana na wizara husika pamoja na taasisi za kitaaluma.
MAJUKUMU YA MAMLAKA
Majukumu ya Mamlaka ni pamoja na:
-
Kuhakikisha upatikanaji wa thamani halisi ya fedha katika ununuzi na ugavi;
-
Kushauri Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi za umma kuhusu kanuni na mbinu za ununuzi na ugavi;
-
Kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu utendaji wa mfumo wa ununuzi wa umma na kupendekeza maboresho;
-
Kudhibiti ununuzi unaohusiana na huduma za ushauri, washauri wa miamala na ushiriki wa sekta binafsi katika miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP);
-
Kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na vyombo vya kitaaluma kuandaa, kusasisha na kutoa nyaraka sanifu za zabuni pamoja na fomu na nyaraka nyingine;
-
Kuidhinisha matumizi ya nyaraka zisizo sanifu za zabuni pale inapohitajika;
-
Kutoa miongozo kwa mujibu wa sheria;
-
Kuanzisha na kusimamia mifumo ya uchapishaji wa taarifa za fursa za zabuni, tuzo za mikataba na taarifa nyingine kwa umma;
-
Kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa kumbukumbu na michakato ya taasisi za ununuzi ili kuhakikisha uzingatiaji wa sheria;
-
Kufuatilia utoaji na utekelezaji wa mikataba ya ununuzi wa umma;
-
Kujenga uwezo kwa wadau wa ununuzi na ugavi; na
-
Kufanya tafiti ndani na nje ya nchi kuhusu masuala ya ununuzi na ugavi.